Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Bw. Tedros Ghebreyesus ametangaza kwamba, janga la homa ya Mpox ni dharura ya afya ya umma duniani.
WHO ilifanya mkutano wa Kamati ya Dharura ya Kimataifa ya Kanuni za Afya (2005) hapo jana ili kujadili kuongezeka kwa maambukizi ya Mpox mwaka huu.
Kulingana na takwimu za WHO, zaidi ya kesi 15,600 za homa ya Mpox zimeripotiwa kufikia sasa mwaka huu, na kuzidi idadi ya kesi mwaka jana, ikiwa ni pamoja na vifo 537.
WHO imesema aina mpya na hatari zaidi ya virusi vya Mpox inaenea kwa kasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na katika nchi jirani za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda, ambazo hazijawahi kuripoti kesi za homa ya Mpox.