Waziri Mkuu wa Ethiopia azindua ujenzi wa mji wa kiuchumi unaotekelezwa na China
2024-08-15 08:59:10| CRI

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezindua ujenzi wa mji wa kiuchumi unaojengwa katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo, Addis Ababa,na kampuni ya China unaojulikana kama “Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Addis ya Kesho.”

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika mwaka mmoja baada ya Utawala wa mji wa Addis Ababa na Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC) kusaini makubaliano ya kujenga mji wa kiuchumi, ambao una ukubwa wa ekari 35, kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 700.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Abiy amesema mji wa kiuchumi ni sehemu ya ahadi ya serikali ya kuufanyia mabadiliko mji wa Addis Ababa kuwa moja ya miji mizuri zaidi duniani kwa kujenga sehemu ya kisasa yenye mambo mbalimbali, ikiwemo nyumba za makazi, maduka makubwa, hoteli na vituo vya burudani.

Naibu meneja mkuu wa kampuni ya CCCC Chen Zhong ameahidi kukamilisha mradi huo kabla ya muda uliopangwa katika njia inayoboresha ushirikiano na uhamishaji wa ujuzi.