Afisa wa Ofisi ya Siasa ya kundi la Hamas Suhail Hindi amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa kundi hilo halitashiriki kwenye mazungumzo kuhusu kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza yatakayofanyika huko Qatar Alhamisi wiki hii.
Amebainisha kuwa kundi la Hamas limetaka Israeli kutoa ahadi wazi ya kufuata makubaliano yaliyofikiwa tarehe pili mwezi Julai, ambayo yalitokana na pendekezo la rais wa Marekani Joe Biden, na kuongeza kuwa kundi hilo liko tayari kushiriki kwenye taratibu za utekelezaji wa makubaliano hayo kama ahadi hiyo itatolewa.
Mazungumzo hayo huko Qatar yaliratibiwa kwa mujibu wa mwaliko wa Misri, Qatar na Marekani yakitarajiwa kutatua masuala yanayofuatiliwa zaidi na msukosuko wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Hapo awali, Hamas iliwataka wapatanishi wa nchi hizo tatu kutoa mpango wa kutekeleza pendekezo la Biden la kusitisha mapigano katika ukanda huo.