Rais wa Kenya William Ruto jana amewapa zawadi ya fedha wanariadha wa nchi hiyo waliopata medali katika michezo ya Olimpiki ya Paris kwa kufanya vizuri katika michezo hiyo.
Katika michezo hiyo, Kenya iliongoza kwa medali barani Afrika kuwa kupata jumla ya medali 11, zikiwemo nne za dhahabu na mbili za fedha.
Rais Ruto alitoa dola za kimarekani 23,256 kwa kila mshindi wa medali ya dhahabu, huku washindi wa medali ya fedha wakipata dola za kimarekani 15,440 na washindi wa medali ya shaba wakipata dola za kimarekani 7,720.
Akizungumza katika hafla ya kupokea timu ya Olimpiki ya Kenya iliyoshiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris iliyofanyika mjini Eldoret, rais Ruto amesema Mfuko wa Michezo umeanzishwa ili kutoa huduma kwa ustawi wa wanariadha na michezo. Ameongeza kuwa, mfuko huo utatumika kushughulika na ustawi wa wanamichezo wanaume na wanawake ambao amewaelezea kuwa ni mabalozi wakubwa wa Kenya.