Mamlaka ya usambazaji wa Umeme vijijini ya Tanzania (REA) imetembelea na kukagua mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji wa Ijangala uliopo Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe na kuahidi kuendelea kuwawezesha waendelezaji binafsi wa umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Bw. Jacob Kingu amepongeza uanzishwaji wa mradi huo ambapo kukamilika kwake kutaongeza Kilowati 360 za umeme katika Gridi ya Taifa.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Endelevu na Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage, amesema kuwa REA imechangia zaidi ya shilingi bilioni 2 katika mradi huo na zaidi ya shilingi bilioni 60 kwa miradi ya waendelezaji binafsi kwa Mkoa wa Njombe, huku akiendelea kutoa wito kwa waendelezaji binafsi kushirikiana na REA kuendeleza miradi yao ili kuongeza umeme katika Gridi ya Taifa.