Sudan kufungua tena mpaka wake na Chad ili kuwezesha misaada ya kibinadamu
2024-08-16 08:43:57| CRI

Baraza la Mamlaka ya Mpito la Sudan limeamua kufungua tena kituo cha Adre kilichoko katika mpaka wa nchi hiyo na Chad kwa muda wa miezi mitatu ili kuruhusu kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Baraza hilo imesema, uamuzi huo umefikiwa jana alhamis katika kikao cha kawaida cha Baraza kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Abdel Fattah Al-Burhan.

Sudan imeshuhudia mapigano makali kati ya Jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha RSF tangu April 15 mwaka jana, na kusababisha vifo vya watu 16,650.

Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, watu milioni 10.7 wamekuwa wakimbizi wa ndani, na wengine milioni 2.2 wametafuta hifadhi katika nchi jirani na Sudan.