Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Bw. Alban Kihulla ametaja fursa kadhaa za uwekezaji unaoweza kufanywa na sekta binafsi katika sekta ya vipimo nchini Tanzania.
Miongoni mwa fursa alizozitaja ni pamoja na sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa mizani mbalimbali na mita za maji, vifaa ambavyo amesema kwa sasa havizalishwi nchini Tanzania bali vinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema kuwa, Sheria ya Vipimo ya Tanzania imeainisha fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta hiyo, na kuongeza kwamba anaamini kupitia sekta binafsi, mita za maji na mizani mbalimbali zinaweza kutengenezwa nchini Tanzania na wakala wa Vipimo ukabaki na jukumu lake la uhakiki wa vipimo hivyo.
Ameongeza kuwa sekta binafsi ikifanyia kazi fursa za uwekezaji alizoziainisha, itasaidia kuongeza nafasi za ajira kwa vijana ambao wanahitimu kutoka vyuo mbalimbali.