Zaidi ya wanafunzi 300 wa vyuo vikuu nchini Ethiopia wamepata ufadhili wa masomo unaotolewa na serikali ya China ili kuwasaidia kuendelea na masomo ya juu katika nyanja mbalimbali za elimu katika vyuo vikuu vikubwa vya nchini China.
Hafla maalum ya kuwaaga wanafunzi hao ilifanyika jana katika Ubalozi wa China nchini Ethiopia na kuhudhuriwa na maofisa wa serikali ya Ethiopia, wanadiplomasia wa China nchini Ethiopia, na familia za wanafunzi waliopata ufadhili huo.
Mkuu wa Dawati la Ufadhili wa Kimataifa katika Wizara ya Elimu nchini Ethiopia Idossa Terfasaa amesisitiza umuhimu wa ongezeko la ufadhili unaotolewa na China kama sehemu ya uhusiano mpana wa nchi hizo mbili katika ujenzi wa uwezo.
Waziri mshauri katika Ubalozi wa China nchini Ethiopia Shen Qinmin ametoa wito kwa wanafunzi hao wa Ethiopia kufanya vizuri katika masomo yao na kutoa mchango halisi kwa maendeleo ya baadaye ya nchi yao.