Agosti Mosi mpaka Agosti 7 ni Wiki ya Kimataifa ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama. Kaulimbiu ya Wiki hii kwa mwaka huu ni “Tatua changamoto: Saidia Unyonyeshaji kwa Watoto”. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, maziwa ya mama yana umuhimu mkubwa sana kwa watoto wachanga, hususan katika miezi sita ya mwanzo ya mtoto. Maziwa ya mama yana virutubisho vyote vinavyotakiwa kwa mtoto, na katika kipindi hicho, sio sahihi kumpa mtoto maziwa ya aina nyingine, iwe ya unga ama ya ng’ombe, kwani maziwa hayo si mazuri kwa afya ya mtoto, kwani mfumo wake wa kumeng’enya chakula bado ni dhaifu.
Lakini unyonyeshaji maziwa ya mama ni muhimu si kwa mtoto pekee, bali pia kwa mama. Wataalamu wanasema, mama anaponyonyesha mtoto wake, anajenga ukaribu kati yake na mtoto, na pia kunyonyesha kunasaidia punguza mama kupata saratani ya maziwa na kupambana na msongo wa mawazo. Kunyonyesha kunaweza kupunguza hatari ya magonjwa kadhaa, pamoja na saratani ya matiti, saratani ya ovari na kisukari cha aina ya 2. Kunyonyesha kwa zaidi ya mwaka, wakati wa maisha ya uzazi wa mwanamke, kunahusishwa na kupunguza 28% ya hatari ya saratani ya matiti na ovari. Wanawake wanaonyonyesha pia wanaweza kufaidika kutokana na hatari ndogo ya shinikizo la damu na ugonjwa wa moyo. Lakini pia inasemekana kuwa, kunyonyesha kunaweza kumsaidia Mama kudhibiti uzito. Katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake, tunaangalia umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto katika miezi sita ya mwanzo ya mtoto.