Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha kwamba historia ya bara la Afrika inarekodiwa kwa usahihi na kulindwa, ili kuondoa dosari za kihistoria.
Akizungumza mjini Harare kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ukombozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Mnangagwa amesema Zimbabwe itaendelea kuwekeza raslimali kwenye masimulizi ya Afrika na mitazamo ya kuondoa fikra za ukoloni kwenye bara hilo.
Amesema wanafahamu kwamba historia ya bara la Afrika imepotoshwa na inaendelea kupotoshwa kwa makusudi, ili kukidhi maslahi ya waliokuwa wakoloni.
Uwanja wa Ukombozi utajengwa kwa awamu kadhaa, ikiwa ni pamoja na jumba la makumbusho ya ukombozi kikiwa ni kivutio kikuu, hoteli ya nyota tano, bustani ya wanyama na makumbusho mengi ya taifa.