Idara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini imewatimua Walibya 95 waliokamatwa kwenye kituo kinachoshukiwa kuwa ni kituo haramu cha mafunzo ya kijeshi nchini Afrika Kusini mwezi uliopita.
Walibya hao 95 walikamatwa na polisi mwezi Julai baada ya kudaiwa kupatikana wakipata mafunzo ya kijeshi katika eneo la White River katika jimbo la Mpumalanga.
Mamlaka ya taifa ya mashtaka ya Afrika Kusini (NPA), hata hivyo Alhamisi iliwafutia mashtaka kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani kwa kukiuka sheria za uhamiaji.
Idara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini imesema kwenye taarifa iliyotolewa jana kuwa imehitimisha jukumu lake la kuwafukuza walibya 95, na kwamba wameondoka kwa ndege iliyolipiwa na Serikali ya Libya.