Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemuhukumu Mussa Shija (32) kifungo cha miaka 20 jela na dada yake Hollo Shija (35) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kujamiiana na maharimu (ndugu wa damu).
Awali, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashitaka ya Taifa Wilaya ya Maswa, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Vedastus Wajanga aliielezea Mahakama kuwa washtakiwa hao ni ndugu wa damu kwa maana ya kaka na dada, waliokuwa wakiishi kama mke na mume na mwaka 2022 walipata mtoto mmoja wa kike.
Alisema ndugu hao wakazi wa Kijiji cha Mandang'ombe wilayani humo walitenda makosa hayo tarehe na miezi tofauti kati mwaka 2018 hadi Julai 31, 2024 katika kijiji hicho.
Washtakiwa hao wakijitetea walisema kuwa waliambiwa na babu yao mzaa baba, kuwa ili wadumishe mila za ukoo wake wanatakiwa wao waoane.