Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) Jumatatu ilitoa utabiri mpya wa hali ya hewa mjini Nairobi nchini Kenya ikisema, huenda eneo la Pembe ya Afrika litakabiliwa na uhaba wa mvua kwenye msimu wa Oktoba hadi Desemba kutokana na hali ya La Nina.
Kwa mujibu wa data kutoka modeli tisa za utabiri duniani, maofisa na wataalamu wanasema hali ya ukame huenda itatokea kwenye sehemu nyingi za eneo hilo kutokana na ongezeko la mvua kati ya Aprili na Julai.
Katibu mtendaji wa IGAD Workneh Gebeyehu amesema mwelekeo wa kunyesha mvua kwenye eneo hilo umekuwa ukisuasua kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni lazima kuchukua hatua za kujiandaa ikiwemo kupanda mazao yanayokomaa haraka.