Zaidi ya wanasayansi 200 kutoka duniani kote wanashiriki kwenye mkutano wa siku nne mjini Nairobi, kujadili njia mpya za kuhimiza biashara ya mbegu zilizoidhinishwa.
Mkutano huo wenye kaulimbiu ya "Uhakikisho wa Ubora wa Mbegu na Maendeleo ya Kiteknolojia Kwa Ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya Tabianchi kuelekea Usalama Endelevu wa Chakula na Lishe", ni wa kwanza kufanyika nchini Kenya, na kutoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu, mafanikio, changamoto na fursa ili kuhimiza biashara ya mbegu bora.
Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo wa Kenya Bw. Andrew Karanja amesema upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo, ni kigezo muhimu cha uzalishaji wa kilimo. Amesema Kenya na nchi nyingine za Afrika zimewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa na huduma za uzalishaji wa mbegu katika miongo miwili iliyopita, na kwamba sekta ya kilimo imekuwa na mchango mkubwa katika usalama wa chakula, ukuaji wa uchumi, na utulivu wa kijamii.