Ukistaajabu ya Musa utayaona ya firauni, mchezaji mmoja ajulikanaye kwa jina la Sebastian Munoz aliamua kujisaidia haja ndogo uwanjani wakati wa mechi ya Copa Peru kati ya Atletico Awajun na Cantorcillo FC. Mchezaji huyo wa Awajun alienda kupiga mpira wa kona, lakini alitakiwa asubiri kwanza kwani kipa wa timu pinzani alikua akipatiwa matibabu.
Baada ya kuona hivyo Munoz akaelekea zege nyuma yake na kujisaidia hapohapo. Mchezaji mwingine wa timu pinzani hakufurahia kitendo hicho na kuamua kwenda kumripoti haraka kwa mwamuzi kama mtoto anayekwenda kumsemea mzazi wake mtu aliyeiba pipi yake. Mwamuzi alimwangalia Munoz, ambaye alikuwa bado anajisaidia pembeni.
Mwamuzi naye hakufurahishwa, hivyo Munoz alionyeshwa kadi nyekundu moja kwa moja. Mwisho wa yote Munoz alifanikiwa kujisaidia, lakini jambo hili litasalia kuwa kama moja ya adhabu ya aibu zaidi katika historia ya soka.