Kongamano la kuunganisha viwango vya usalama wa chakula na kuimarisha biashara ya kilimo barani Afrika lafanyika Nairobi
2024-08-21 09:07:40| CRI

Wataalamu wamekogamana mjini Nairobi, kujadili namna ya kuoanisha viwango vya usalama wa chakula na kuharakisha biashara ya kilimo barani Afrika .

Kongamano hilo la siku mbili limewakutanisha wataalam zaidi ya 200, wanaofanya mapitio kuhusu ushirikiano kati ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kuunda mfumo wa viwango vya kimataifa vya chakula ili kuimarisha biashara barani Afrika.

Ofisa wa Shirika la Viwango nchini Kenya (KEBS) Bibi Maryann Kindiki, kutoka idara inayoshughulikia utekelezaji wa viwango vya pamoja vya chakula vya FAO na WHO, amesema viwango tofauti vya kitaifa vya usalama wa chakula, vinaleta vizuizi vya kiufundi kwa biashara ya barani Afrika, hasa bidhaa za kilimo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Afrika gharama ya uagizaji wa chakula barani Afrika inakadiriwa kuwa dola za kimarekani bilioni 60 kwa mwaka, licha ya bara hilo kuwa na asilimia 60 ya ardhi inayolimika duniani.