Mgomo wa Walimu Kuanza Jumatatu Baada ya TSC Kushindwa Kutimiza Matakwa
2024-08-22 10:24:38| cri

Shughuli za masomo zitatatizwa kote nchini Kenya iwapo walimu watatekeleza tishio lao la kuanza mgomo.

Shule zinatarajiwa kufunguliwa tena kwa muhula wa tatu Jumatatu, Agosti 26. Vyama vitatu vya walimu vilikutana na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Jumatano, Agosti 21, kutatua mkwamo huo, lakini juhudi zao ziligonga mwamba. Muungano wa Kitaifa wa Walimu nchini humo (KNUT), Muungano wa Walimu wa Shule za Upili (KUPPET), na Muungano wa Walimu wa Elimu ya Mahitaji Maalum (KUSNET) wameazimia kufanya mgomo wa kitaifa kuanzia Jumatatu.