Mvua kubwa na mafuriko vyawaua watu 114 nchini Sudan kuanzia mwezi Juni
2024-08-22 08:48:32| CRI

Wizara ya afya ya Sudan imeripoti kuwa mvua kubwa na mafuriko katika msimu wa mvua ulioanza mwezi Juni, vimesababisha vifo vya watu 114.

Ofisi ya mambo ya dharura ya wizara hiyo imesema katika taarifa yake kuwa idadi ya watu waliofariki imeongezeka hadi kufikia 114, na wengine 281 wamejeruhiwa. Majimbo kumi yameathiriwa, na kuathiri familia 27,278 na watu 110,278.

Tarehe 10 Agosti wizara hiyo iliripoti vifo 53 na majeruhi 208 kutokana na mafuriko na mvua katika majimbo tisa kati ya mwezi Juni na Julai.

Mafuriko ni tatizo linalotokea mara kwa mara nchini Sudan kati ya mwezi Juni na Oktoba. Mvua kubwa za hivi karibuni zimesababisha hasara kubwa ya maisha na uharibifu wa ardhi ya kilimo.

Msimu wa mvua wa mwaka huu umezidisha msukosuko wa kibinadamu nchini Sudan, ambayo inakabiliwa na mgogoro mkubwa kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na vikosi vya Msaada wa Haraka.