Waziri mkuu wa China Bw. Li Qiang Alhamisi alikutana na rais Alexander Lukashenko wa Belarus kwenye Ikulu ya Belarus mjini Minsk.
Kwenye mazungumzo yao, Li alisema katika miaka 32 tangu China na Belarus zilipoanzisha uhusiano wa kibalozi, uhusiano kati ya nchi mbili unaonyesha nguvu ya uhai. Pande mbili zinashikilia ushirikiano wa kunufaishana na kupata maendeleo kwa pamoja, na ushirikiano wa kiutendaji umepata matunda mengi na kuwanufaisha wananchi wa nchi mbili.
Mwezi Julai mwaka huu, wakuu wa nchi hizo mbili walikutana huko Astana, ambako waliweka mpango wa kimkakati juu ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili. China inapenda kushirikiana na Belarus katika kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi mbili, kuendelea kuimarisha uaminifu wa kisiasa, kuongeza zaidi ushirikiano wa kunufaishana, kuhimiza uhusiano wa siku zote wa wenzi wa kimkakati katika pande zote kati ya nchi mbili upate maendeleo ya kiwango cha juu, na kuwanufaisha zaidi wananchi wa nchi hizo mbili.
Kwa upande wa Belarus, Lukashenko alisema kwa sasa maendeleo ya uhusiano kati ya Belarus na China yana mwelekeo wenye nguvu, hali ambayo iko juu zaidi kihistoria, nchi mbili siku zote zinaungana mkono kithabiti juu ya masuala makubwa yanayohusiana na maslahi makuu. Belarus inaishukuru China kwa kutoa msaada kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Belarus kwa muda mrefu. Belarus inapenda kudumisha mawasiliano ya ngazi ya juu na China, na kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji kwenye sekta za uchumi, biashara, kilimo, sayansi na teknolojia.