Mjumbe wa China asema mazungumzo ya kusitisha vita na suluhisho la kisiasa ni njia ya msingi kutatua mgogoro kati ya Palestina na Israel
2024-08-23 10:04:10| CRI

Mjumbe wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Fu Cong amesema kwenye mkutano wa Baraza la Usalama juu ya suala la Palestina na Israel kuwa wazo la kutaka kupata ushindi katika Ukanda wa Gaza kupitia operesheni za kijeshi linaweza kusababisha vifo na majeruhi ya raia wengi zaidi badala ya kutoa fursa kuwaokoa waliotekwa na kuleta utulivu na amani kwa Israel na kanda hiyo. Amesisitiza kuwa mazungumzo ya kusitisha vita na suluhisho la kisiasa ni njia ya msingi kutatua mgogoro huo.

Balozi Fu amesema China inaitaka Israel isitishe operesheni zote za kijeshi katika Ukanda wa Gaza pamoja na hatua zinazochochea mivutano ya kikanda, huku ikizitaka nchi zenye ushawishi mkubwa ziwe wadhati na kutenda haki na kubeba majukumu yao katika suala hilo. Amesema China itaendelea kuunga mkono Baraza la Usalama katika hatua zake za kutekeleza maazimio husika na kusitisha vita katika Ukanda huo.