Kenya yapeleka wanajeshi kulinda utulivu DRC
2024-08-26 09:28:14| CRI

Jeshi la ulinzi la Kenya KDF limesema kundi la kwanza la kikosi cha 4 cha mwitikio wa haraka cha Kenya (KENQRF 4) liliondoka kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Jumamosi ili kuungana na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO kinachobeba jukumu la kutuliza vurugu kubwa zinazochochewa na makundi yenye silaha mashariki mwa nchi hiyo.

Kamanda wa Kambi ya Jeshi la Anga ya Embakasi Stephen Kapkory jana alitoa taarifa jijini Nairobi akieleza imani yake na kiwango cha mafunzo na taaluma cha wanajeshi hao na kuwataka wawe mabalozi wazuri wa Kenya kwa kudumisha weledi na nidhamu ya hali ya juu katika shughuli hiyo.

Kwa mujibu wa KDF, kutumwa kwa wanajeshi hao wa Kenya kunakuja wakati ambapo MONUSCO imezidisha juhudi zake katika kulinda raia, kuboresha sekta ya usalama, na kupokonya silaha, kuwaondoa wapiganaji na kuwajumuisha tena kwenye jamii.