Mkurugenzi wa ofisi ya mawasiliano ya serikali wa wilaya ya Telemet Bw. Tesfaye Workneh ametoa taarifa akisema, maporomoko ya udongo yaliyotokana na mvua kubwa yamesababisha vifo vya watu 10 na wengine wanane kujeruhiwa Jumamosi katika wilaya ya Telemet jimboni Amhara, kaskazini mwa Ethiopia.
Workneh amebainisha kuwa hadi sasa miili minne imegunduliwa, na wenyeji na timu za uokoaji wanaendelea kutafuta mingine sita ambayo haijapatikana. Maporomoko ya udongo pia yamesababisha vifo vya ng’ombe 35, huku hekta 30 za mazao yaliyoko shambani zikiharibiwa.
Ameongeza kuwa watu 2,400 kutoka kaya 480 wamepoteza makazi yao kutokana na maporomoko ya udongo. Alitoa rai kwa wakazi wa huko kuchukua tahadhari kwa mafuriko na maporomoko ya udongo yanayoweza kutokea katika maeneo ya karibu.