Serikali ya Tanzania inatarajia kutangaza fursa za kiuchumi kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi zitokanazo na mazingira ili kuokoa maliasili ambazo zimeharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Ashatu Kijagi, alipozungumza na wanahabari kuhusu maandalizi ya mkutano wa viongozi, wataalamu na wadau kuhusu uhifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema mkutano huo utajadili fursa zilizopo katika hifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na Biashara ya Kaboni; usimamizi wa taka; mabadiliko ya tabianchi; nishati safi ya kupikia; upandaji miti na usimamizi na ufuataji wa Sheria nchini humo.