Watu 25 waliuawa na wengine 30 kujeruhiwa katika shambulio la silaha lililofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) siku ya Jumatatu huko El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini magharibi mwa Sudan.
Akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua, mkuu wa afya wa Jimbo la Darfur Kaskazini, alisema RSF ililenga soko la kambi ya Abu Shouk kwa makombora manne Jumatatu, yaliyosababisha watu 25 kuuawa na wengine 30 kujeruhiwa. Majeruhi wamepelekwa katika vituo vya afya katika eneo la Abu Shouk, Hospitali ya Saudia, na hospitali ya jeshi.
Kamati ya upinzani ya El Fasher, kundi lisilo la kiserikali, ilisema katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook siku ya Jumanne kwamba RSF Jumatatu ilishambulia Chuo binafsi cha Kusini mwa Sahara huko El Fasher, na kuharibu ukumbi wake mkuu, maabara, chumba cha kuhifadhi maiti na majengo mengine.
Hadi sasa RSF bado haijasema chochote kuhusiana na matukio hayo.