Viongozi sita kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zikiwemo Burundi, Kenya, Sudan Kusini, Uganda, Tanzania na Rwanda Jumanne waliahidi kuunga mkono azma ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), na kusema Odinga ndiye mgombea anayefaa zaidi kwa nafasi hiyo ya bara.
Akizungumza wakati wa kuzindua rasmi azma ya Odinga katika AUC huko Nairobi, Kenya, Rais wa Kenya William Ruto alisema Odinga ni kiongozi mwenye maono na ana uwezo wa kitaaluma na uzoefu unaomfanya kuwa mgombea bora wa kuongoza AUC. Kiongozi huyo wa Kenya pia alisema jukumu hilo katika AUC ni kazi nzuri inayolenga kuleta uhuru na demokrasia, utulivu na usalama, amani na ustawi.
Kiti cha mwenyekiti wa AUC kinatarajiwa kuwa wazi ifikapo Februari 2025 kwani anayekalia sasa, Moussa Faki wa Chad, anatarajiwa kumaliza awamu yake ya pili. Faki aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na alishinda awamu ya pili mwaka 2021.