Rais wa Zanzibar awatunuku nishani timu ya madaktari wa China
2024-08-28 09:38:05| CRI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amewatunuku wajumbe wa  timu ya 33 ya madaktari wa China nishani na vyeti vya kumbukumbu kwa kutambua mchango wao katika shughuli za matibabu na afya nchini Tanzania.

Hafla ya kutoa nishani hizo ilifanyika Jumatatu katika Ikulu ya Zanzibar baada ya timu hiyo kumaliza huduma za matibabu za mwaka mmoja visiwani humo. Dkt Mwinyi aliishukuru serikali ya China kwa mchango wake mkubwa  kwa ajili ya huduma za matibabu na afya Zanzibar katika miaka 60 iliyopita, na kuipongeza timu ya madaktari wa China kwa juhudi kubwa na dhamira yao ya kujitolea.

Amesema timu ya madaktari wa China  pia walifanya matibabu kwa vifaa vya teknolojia ya hali ya juu katika kutibu wagonjwa visiwani humo na kutoa mafunzo kwa madaktari wenyeji na wanafunzi wenyeji wa somo la udaktari ili  kuandaa vipaji na kuendeleza sekta ya afya Zanzibar.

Naye mkuu wa timu ya madaktari wa China, Jiang Guoqing, alisema timu ya madaktari wa China itaendelea kuimarisha ushirikiano na mawasiliano kwenye masuala ya afya na Zanzibar, kutoa huduma za matibabu za hali ya juu kwa wenyeji, na kutoa mchango mkubwa zaidi  kwa ajili ya urafiki kati ya China na Afrika. Timu hiyo iliwasili Zanzibar Septemba mwaka jana, na kuwahudumia wagonjwa karibu 40,000, na kutoa matibabu ya bure kwa mara 20 kisiwani humo.