Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Jumatano alimpongeza Faustine Engelbert Ndugulile kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika akimrithi Matshidiso Moeti, ambaye ameshika wadhifa huo tangu mwaka 2015.
Ndugulile ambaye ni Waziri wa zamani wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Naibu Waziri wa zamani wa Afya, alichaguliwa Jumanne wakati wa kikao cha 74 cha Kamati ya WHO ya Kanda ya Afrika huko Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, baada ya kuwashinda Boureima Hama Sambo wa Niger, Richard Mihigo wa Rwanda, na Ibrahima Soce Fall wa Senegal.
Mkuu huyo wa nchi alisema Ndugulile ameifanya Tanzania kujivunia, na Bara la Afrika litafaidika sana na kazi yake, na ana imani kuwa utaalamu na uzoefu wake katika sekta ya afya utaiwezesha Afrika kuwa na sauti muhimu katika ngazi ya kimataifa katika kukabiliana na changamoto za kiafya kwa mamilioni ya watu wa bara zima.
Ndugulile amechaguliwa katika nafasi hiyo huku kukiwa na magonjwa ya mlipuko katika bara la Afrika, ukiwemo wa hivi karibuni wa mpox.