Wataalamu wakutana nchini Kenya kujadili namna ya kuimarisha matumizi ya mbolea barani Afrika
2024-08-29 09:04:02| CRI

Wataalamu mbalimbali wamekutana Nairobi, Kenya siku ya Jumatano ili kujadili njia za kuongeza matumizi ya mbolea miongoni mwa wakulima barani Afrika.

Warsha hiyo ya siku tatu baada ya Mkutano wa Kilele wa Mbolea na Afya ya Udongo wa Afrika, iliwaleta pamoja wajumbe zaidi ya 100 kutoka Umoja wa Afrika (AU), jumuiya za kiuchumi za kikanda, watafiti pamoja na maafisa wa serikali kutoka Afrika ili kuimarisha matumizi ya mbolea na usalama wa chakula barani humo.

Mshauri mwandamizi katika Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika wa Kamisheni ya AU, Panduleni Elago alisema matumizi ya mbolea miongoni mwa wakulima wadogo, ambao ndio wengi barani Afrika na kulima sehemu kubwa ya ardhi, yameongezeka katika muongo mmoja uliopita, lakini bado ni ya chini ya kiwango kinachohitajika kwani wakulima wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazopunguza mahitaji yao ya mbolea.

Naye Mkurugenzi wa sekta za uzalishaji katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jean Baptiste Havugimana alisema Bara la Afrika limeanzisha programu nyingi ukiwemo Utaratibu wa Kufadhili Mbolea Afrika, mfuko maalum unaolenga kuboresha uzalishaji wa kilimo kwa kutoa fedha zinazohitajika kuongeza matumizi ya mbolea barani Afrika ili kufikia lengo la kilo 50 za virutubisho kwa hekta.