Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kwamba hali ya kibinadamu katika majimbo mengi ya Sudan Kusini inazidi kuzorota kwa kasi, huku kukiwa na usumbufu mkubwa katika ufikishaji wa misaada muhimu kwa watu walio hatarini.
Kwenye taarifa yake mpya iliyotolewa Jumatano huko Juba, Sudan Kusini, OCHA ilisema kuwa usalama wa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu upo kwenye tishio kubwa kutokana na kuongezeka kwa utekaji nyara na ghasia.
Hata hivyo limesema ingawa idadi ya matukio ilipungua kidogo Julai ikilinganishwa na mwezi uliopita, kupungua huku kumechangiwa zaidi na mwanzo wa msimu wa mvua, na kuwawekea vikwazo vikali wafanyakazi na usafirishaji wa misaada barabarani.Ilisema washirika wa kibinadamu waliripoti matukio 34 mwezi Julai pekee, ikionesha hali ya kutisha na inayoendelea kutoka mwaka uliopita.