Shirika la Msalaba Mwekundu la Kimataifa(ICRC) limesema zaidi ya watu 71,000 hawajulikani walipo kwa sasa barani Afrika, ikiashiria ongezeko la asilimia 75 tangu 2019 kutokana na vita, ghasia, majanga ya asili na uhamiaji.
Kabla ya Siku ya Kimataifa ya Kutoweka inayoadhimishwa Agosti 30, mkurugenzi wa ICRC kanda ya Afrika Patrick Youssef alisema katika taarifa iliyotolewa jijini Nairobi kuwa wakati kila mtu anapopotea, kuna wengi wanaopitia mateso makubwa yasiyohesabika kutokana na uchungu na kutokuwa na uhakika. Ni janga la kibinadamu kwa familia, ambalo pia lina madhara kwa jamii nzima.
Youssef alisema kuwa suala la kupotea kwa watu, ikiwa ni pamoja na wale waliolazimishwa kutoweka, limekuwa moja ya athari mbaya na za kudumu za kibinadamu zinazotokana na migogoro na ghasia. Kwa mujibu wa matukio yaliyosajiliwa na ICRC hadi kufikia mwezi Juni, Afrika ina idadi kubwa zaidi ya watu waliopotea, watoto wasio na walezi na kuunganishwa tena kwa familia.