Kenya yazindua mpango wa kukuza sekta ya mafao ya kustaafu
2024-08-30 09:43:33| CRI

Kenya Alhamisi ilizindua mpango mkakati unaolenga kukuza sekta jumuishi na endelevu ya mafao ya kustaafu.Akiongea na wanahabari mjini Nairobi, Kenya, Katibu mkuu katika Wizara ya Fedha na Mipango ya Uchumi, Chris Kiptoo, alisema Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mamlaka ya Mafao ya Kustaafu unalenga kukuza akiba ya wastaafu kutoka shilingi trilioni 1.7 (kama dola bilioni 13.2 za Kimarekani) hadi dola bilioni 24.8 kufikia mwaka 2029.

Kiptoo alisema mwongozo huo pia unaelezea hatua za kupanua malipo ya pensheni kutoka asilimia 26 ya sasa ya wafanyakazi hadi asilimia 34 ifikapo 2029.Alisema kuwa malipo ya mafao ya kustaafu yameendelea kuwa ya chini, hasa kutokana na muundo wa soko la ajira nchini Kenya, ambapo takriban asilimia 85 ya wafanyakazi wameajiriwa katika sekta isiyo rasmi, na kufanya uwekaji akiba wa kustaafu kuwa si wa kawaida.