Shirika la Kuhudumia Wakimbizi na Waliorejea nchini la Ethiopia (RRS) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Alhamisi walitangaza kuanzishwa kwa eneo jipya huko Amhara nchini Ethiopia kwa ajili ya watu wanaokimbia machafuko katika nchi jirani ya Sudan.
Katika taarifa yake RRS imesema Kuanzishwa kwa eneo hilo jipya linalojulikana kama Aftit kulikuja baada ya kufungwa kwa maeneo mengine mawili, Awlala na Kumer, ambapo sasa limeimarishwa usalama kwa kushirikiana na serikali za mitaa na jamii kwa ajili ya ulinzi bora wa wakimbizi. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa kuwa RRS, UNHCR na washirika wengine wameendelea kutoa huduma bora zaidi zikiwemo msaada wa chakula, maji safi, huduma za usafi wa mazingira, misaada ya matibabu na ulinzi kwa wakimbizi katika eneo jipya.
Takriban wanaume, wanawake na watoto 3,000 walisafirishwa hadi Aftit, wakati mamia kadhaa ya wengine ambao walikuwa wanakaa katika maeneo tofauti ndani ya mkoa wa Amhara wamehamia katika eneo jipya, ambalo linaweza kuchukua hadi watu 12,500.