Tanzania ipo tayari kuendeleza nishati ya nyuklia
2024-08-31 22:54:16| cri

Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema nchi hiyo imeandaa mpango wa uendelezaji wa nishati ya nyuklia, ikiwa ni moja ya vyanzo mbadala vya nishati safi ya umeme kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Dk. Biteko amesema hayo wakati akiwasilisha Mpango wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Masuala ya Nishati ya Nyuklia kati ya Marekani na nchi za Afrika unaoendelea Jijini Nairobi, nchini Kenya.

Katika mkutano huo, Dk. Biteko amesema Tanzania iko tayari kuendeleza nishati ya nyuklia ikiwa ni moja ya vyanzo vitakavyoiwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika na ambayo inakidhi viwango vya kimataifa katika uhifadhi wa mazingira.

Amesema mahitaji ya umeme nchini Tanzania yanaongezeka kwa asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka, na ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, Tanzania imepanga kuzalisha megawati 10,000 za umeme ifikapo mwaka 2030.