Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwaongoza mawaziri zaidi ya 70 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), watakaokutana nchini Tanzania kujadili masuala mbalimbali ya uchumi wa bluu ili kuweka mkakati wa pamoja kuimarisha sekta ya uvuvi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania Bw. Abdallah Ulega, amewaambia wanahabari kuwa mkutano huo utafunguliwa na Dk. Samia Suluhu Hassan Septemba 11 na umepangwa kufanyika sambamba na Kongamano la Kimataifa linalohusu mikakati ya Uboreshaji wa Mnyororo wa Uzalishaji wa Vyakula vya Majini ulioandaliwa na Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani (FAO).