Chama tawala cha Tanzania CCM kimesema kina matarajio makubwa na mkutano wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaotarajiwa kufanyika mwezi Septemba mjini Beijing.
Akiongea mjini Beijing na China Media Group, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (CCM–NEC) anayeshughulikia mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Bi。 Rabia Abdalla Hamid, amesema Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kushiriki kwenye mkutano huo, na Tanzania inatarajia kuwa ajenda zinazohimizwa na serikali ya Rais Samia Suluhu kwenye kutatua changamoto na kuboresha maisha ya watanzania, zitakuwa sehemu ya mkutano wa FOCAC. Bi Rabia amesema,
“Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano wa FOCAC, na kwenye mkutano huu tunajua ni ajenda gani ambazo Rais Samia anazifuatilia zaidi ambazo pia zinafuatiliwa na dunia nzima, ambazo ni pamoja na biashara ya kimataifa, miundo mbinu, nishati mpya, kuna ajenda maalum pia ambazo Rais Samia anazipigania zaidi za kuokoa maisha ya watanzania, kama vile ajenda ya mama na mtoto na kupunguza vifo watoto wanaozaliwa, tunaamini kuwa Rais Samia ataendelea kufuatilia ajenda hizo. Kwa kuwa China ni nchi inayofamika sana kwenye maeneo hayo, tunaamini kuwa kutakuwa na matokeo chanya”.
Bi. Rabia pia ametoa maoni kuhusu juhudi za China katika kuiendeleza nchi kuwa ya kisasa kwa mtindo wake, na huku ikiendelea kulinda utamaduni wa China. “ninawaelewa vizuri wachina wanapotaja kuifanya China kuwa ya kisasa kwa mtindo wa China yenyewe. Vigezo vya kuleta mambo ya kisasa vinatofautiana kati ya nchi na nchi. Kwa hiyo tunaweza kuangalia ni vipi vinaendana na sisi. Sioni ubaya wowote kwenye kusema nataka kuwa wa kisasa lakini sitaki kuacha maadili yangu”.
Bi. Rabia pia amekumbusha kuwa Rais Samia pia anaendelea na juhudi za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kisasa lakini bila kusahau maadili ya mtanzania. Amesema, “Tanzania nayo inafanya juhudi za kuwa nchi ya kisasa, na Rais wetu Dk. Samia anapigania kuifungua nchi yetu na kutaka iwe ya kisasa, kwa hiyo tunaunga mkono wazo hilo la kufanya nchi kuwa ya kisasa. Sisi tunachoweza kujifunza ni vipi wachina wanaweza kujiendeleza kuwa nchi yao kuwa kisasa wakati inaendelea kubaki na utamaduni wao”.
Wakati China ikijiandaa kukaribisha viongozi kutoka nchi mbalimbali kwenye mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, wanazuoni wa mambo ya ushirikiano kati ya China na Afrika wamekuwa wakijadili kuhusu ukaribu kati ya pande hizi mbili, na jinsi dhana za ushirikiano na maendeleo kati ya pande hizi mbili zinavyoshabihiana. Bi. Rabia anasema,
“China inasema ‘kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja’, na Rais wetu amekuwa akisema ‘ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako’. Hii ina maana kuwa Tanzania na China zinakubaliana kwenye hiyo dhana ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja, yaani kusonga mbele kwa pamoja. Na unapoalika nchi kwenye mkutano kama huu wa FOCAC, kujadili mambo ya ushirikiano na unaowaalika wanakubali kuja, hii ina maana kuwa mna ajenda zinazofanana. Unaweza kuwaalika watu lakini wasitokee, lakini pia unaweza kutoamua kuwaalika kama huna ajenda inayofanana na yule unayemwalika. Kwa hiyo watu wenye ajenda zinazofanana wanafanya kazi kwa pamoja, au ndege wanaoruka pamoja, ni wale wanaofanana.”