Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini China kuanzia tarehe 2 hadi 6 Septemba, na kushiriki kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing.
Taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya Ikulu ya Tanzania, imesema wakati wa ziara yake rais Samia atakutana na mwenyeji wake Rais Xi Jinping, na kufanya mazungumzo yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China ulioanza miaka 60 iliyopita.
Marais hao wawili pamoja na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema, pia watashiriki na kushuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano ya kuboresha Reli ya TAZARA.
Rais Samia pia anatarajiwa kuwa miongoni mwa wakuu wa nchi watakaohutubia ufunguzi wa Mkutano wa FOCAC, akizungumza kwa niaba ya Kanda ya Afrika Mashariki.
Pembezoni mwa mkutano huo, Rais Samia atakutana na makampuni na wawekezaji kutoka China kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini Tanzania.