Tanzania yaruhusiwa kuuza maparachichi kwenye soko la China
2024-09-02 14:56:14| cri

Ni furaha kwa wakulima wa parachichi nchini, baada ya Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), kufanikiwa kufungua soko la parachichi nchini China.

Ruhusa hiyo imetokana na itifaki ya usafi na udhibiti wa magonjwa ya mimea iliyosainiwa mwaka 2022 kati ya Tanzania na China, ikiruhusu maparachichi ya Tanzania kuuzwa kwenye soko la China. Mbali na maparachichi, soko la mbegu za alizeti pia limefunguliwa nchini China, likiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kilimo kati ya nchi hizi mbili.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hatua hiyo itapanua wigo wa biashara ya maparachichi na kuwasaidia wakulima wa Tanzania kukuza uchumi kupitia zao hilo. Kufunguliwa kwa soko la China pia kunaiwezesha Tanzania kuimarisha zaidi soko la kimataifa la parachichi baada ya kufanikiwa kuteka masoko mengine barani Ulaya kama Denmark, Ufaransa, Uholanzi, Norway, Hispania, na Uingereza.