Rais Xi Jinping ashiriki kwenye shughuli za pande mbili na viongozi wa nchi za Afrika waliowasili Beijing kuhudhuria mkutano wa FOCAC 2024
2024-09-02 15:26:00| cri

Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika wa mwaka 2024 utafanyika Septemba 4 hadi 6 hapa Beijing. Viongozi wa China na Afrika watajumuika mara nyingine tena kukuza urafiki, kujadili ushirikiano na kupanga siku zijazo za uhusiano kati ya China na Afrika, chini ya kaulimbinu ya “Kushikana Mikono Kuelekea Kuwa Nchi za Kisasa, Kujenga kwa Pamoja Jumuiya ya Kiwango cha Juu yenye Hatma ya Pamoja Kati ya China na Afrika”.

Rais Xi Jinping wa China atahudhuria na kuhutubia ufunguzi wa mkutano huo Septemba 5. Katika kipindi cha mkutano huo, Rais Xi pia ataandaa tafrija ya kuwakaribisha viongozi wa nchi za Afrika na wajumbe kutoka mashirika ya Afrika na ya kimataifa na shughuli nyingine za pande mbili.

Leo Septemba 2, Rais Xi amekutana na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Bw. Felix Tshisekedi, ukiwa ni mkutano wa kwanza wa pande mbili kati ya Rais Xi na viongozi wa nchi za Afrika walioko Beijing kuhudhuria mkutano wa FOCAC.