Rais Xi Jinping wa China leo asubuhi katika Jumba Kuu la Mikutano ya Umma mjini Beijing amekutana na mwenzake wa Kenya Willam Ruto ambaye amekuja China kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Akipongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ushirikiano kati ya China na Kenya hasa kwenye ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, Rais Xi amependekeza pande hizo mbili kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati kwa kuelekea nyanja tatu. Kwanza ni kuenzi na kueneza urafiki, kuaminiana na kuungana mikono katika kutafuta njia ya maendeleo inayofaa hali halisi; Pili ni kuendeleza ushirikiano wa kunufaishana na kuunganisha kwa karibu ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na “Ruwaza ya 2030” ya Kenya; Tatu ni kushirikiana kimkakati katika kulinda haki na usawa, kuimarisha uratibu na mawasiliano kwenye masuala ya kikanda na kimataifa, kuungana mikono katika kulinda maslahi ya pamoja ya Nchi za Kusini duniani, na kuhimiza amani na utulivu wa kikanda.
Rais Ruto ameishukuru China kuandaa Mkutano huu wa FOCAC, ambao utatoa jukwaa na fursa kwa Afrika na China kutafuta maendeleo katika siku zijazo. Amesema uhusiano kati ya Kenya na China umejengwa katika msingi wa urafiki mkubwa, kuheshimiana, kuaminiana na kunufaishana. Amesema Kenya itafuata kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja duniani, na inapenda kushirikiana kwa karibu na kuungana mkono kithabiti na China.