Mawasiliano na ushirikiano katika sekta ya lugha kati ya China na Afrika ni muhimu kwa uunganishaji wa mioyo ya watu kati ya pande hizo mbili
2024-09-03 09:47:43| CRI

Mkutano wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utafanyika wiki hii hapa Beijing. Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Dkt. Caroline Asiimwe ambaye alikuwa nchini China kushiriki katika shughuli za vyombo vya habari za “Wenzi wa Afrika”, amesema katika mahojiano na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) kuwa, mawasiliano na ushirikiano wa sekta ya lugha kati ya China na Afrika yanasaidia kuunganisha mawasiliano ya watu kati ya pande hizo mbili.

Mwaka 2021 Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO ulitangaza Julai 7 kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Kiswahili ikiwa lugha ya kienyeji ya Afrika, mashirika ya kimataifa na wadau wa sekta mbalimbali wanajitahidi kuhimiza umhimu wake katika mawasliano, na hivi sasa Kiswahili kimetambuliwa kuwa lugha muhimu ya kuhimiza mshikamano na amani ya kikanda.

Dkt. Asiimwe amesema amefurahi kuona kuwa China pia inafanya juhudi za dhati za kukuza lugha ya Kiswahili, na kama mwakilishi wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, anaona kuwa shughuli hizo ni mwanzo wa ushirikiano na mawasiliano kati ya CMG na nchi za Afrika katika ushirikiano wa lugha ya Kiswahili.

Wakati huo huo, amesema mbali na ushirikiano kati ya vyombo vya habari, vyuo vikuu vingi vimeanzisha kozi ya lugha ya Kiswahili. Anaamini kuwa mawasiliano na ushirikiano wa sekta ya lugha na utamaduni ni muhimu sana, kwa kuwa lugha inagusa mioyo ya watu, na utamaduni unahusiana na maisha ya watu.

Mawasiliano na ushirikiano katika sekta ya lugha kati ya China na Afrika yanawasaidia watu wa China na Afrika kuelewana vizuri na kuwafanya kuwa karibu zaidi, na kuhimiza ushirikiano kukita mizizi katika mioyo ya watu wa pande hizo mbili.

Akizungumzia Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika utakaofanyika wiki hii Dkt. Asiimwe anatarajia kuwa mkutano huo utafikia makubaliano zaidi ili kuchangia maendeleo na kuwanufaisha zaidi watu wa pande hizo mbili.