Kenya itakuwa mwenyeji wa toleo la saba la Maonyesho ya Kimataifa ya Viwanda yatakayofanyika wiki ijayo, ambayo yanalenga kuboresha uhusiano kati ya China na Afrika.
Mkurugenzi mtendaji wa Afripeak Expo Kenya amewaambia wanahabari jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya, kwamba maonyesho hayo ya siku tatu yataanza Septemba 12 na yatakutanisha zaidi ya washiriki 200 kutoka China na Afrika watakaoonyesha bidhaa zao mpya.
Amesema maonyesho hayo yatakuwa jukwaa la kuunganisha wawekezaji wa China na Afrika ili kuwezesha mabadilishano ya ujuzi na matumizi ya teknolojia mpya ili kuboresha ushindani wa viwanda vya barani Afrika.
Meneja mkuu wa Kuhamasisha Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara katika Mamlaka ya Uwekezaji ya Kenya Pius Rotich amesema, maonyesho hayo yatajumuisha watengenezaji wa vipuri vya magari, ujenzi wa miundombinu, mashine za kilimo, vifaa vya ujenzi, nishati mpya na bidhaa za mazingira na kemikali.