Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema ni muhimu kuwa na usawa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku akieleza Tanzania imeendelea kusisitiza ujumuishaji wa masuala ya jinsia na mabadiliko kupitia sera, programu na mikakati kwenye ngazi zote.
Dk Mpango amesema hayo mjini Arusha wakati wa ufunguzi wa baraza la 24 na mkutano wa 35 wa kamati ya kudumu ya fedha ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC). Amesema ni muhimu kufanywa jitihada za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo athari zake zimejitokeza katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula, afya na ikolojia, huku wanawake, vijana na watoto wakiwa ni wahanga wakubwa zaidi.
Dk Mpango amesema dunia inasubiri ripoti za tathmini na muhtasari wa fedha za masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, na ripoti ya maendeleo kuhusu upatikanaji wa Dola bilioni 100 za Marekani ili kufanikisha utekelezaji wa mkataba wa Paris, kwenye kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.