AfDB yapokea dola milioni 151 za kimarekani kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika
2024-09-03 09:05:10| CRI

Mfuko wa Kijani wa Hali ya Hewa unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa umeidhinisha ufadhili wa dola za kimarekani milioni 151 kusaidia program kubwa ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika Pembe ya Afrika.

Program hiyo inayoungwa mkono na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), itasaidia mradi wa Benki hiyo wa “Kujenga Unyumbufu kwa ajili ya Chakula na Maisha katika Pembe ya Afrika,” na kunufaisha watu milioni 4.6 katika nchi za Djibouti, Somalia, Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini.

Mkurugenzi wa Kilimo na Kilimo cha Kibiashara wa Benki hiyo Martin Fregene amesema, kupatikana kwa fedha hizo kunaonyesha mwendelezo wa Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika kuongeza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na mifumo endelevu ya kilimo katika Pembe ya Afrika, na hivyo kuboresha usalama wa chakula katika moja ya maeneo yaliyoko hatarini zaidi duniani.