Rais Xi Jinping wa China leo amekutana na mwenzake wa Tanzania rais Samia Suluhu Hassan ambaye yuko Beijing kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa mwaka 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC.
Rais Xi ameeleza kuwa mwaka huu ni wa maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania, hivyo China inapenda kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha kwa kina ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili ili kuwanufaisha wananchi wa nchi mbili na urafiki wa jadi kati ya China na Tanzania uweze kuenziwa kizazi hadi kizazi. Amesema China inapenda kutumia Mkutano huo kama fursa ya kuhimiza maendeleo mapya katika ufufukaji wa Reli ya TAZARA, kushirikiana kuboresha mtandao wa usafiri wa reli na baharini wa Afrika Mashariki, na kuijenga Tanzania kuwa eneo la mfano la kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika katika kujenga kwa pamoja "Ukanda Mmoja, Njia Moja".
Rais Xi pia amesisitiza kuwa China inapenda kushirikiana na Tanzania kujenga uhusiano kati ya nchi hizi mbili kuwa mfano wa uhusiano kati ya China na Afrika na ushirikiano wa Kusini na Kusini, na kutoa mchango mkubwa zaidi katika kukuza ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu.
Kwa upande wake rais Samia alieleza furaha yake ya kuja tena China baada ya mwaka 2022 na kuhudhuria mkutano wa kilele wa Beijing wa FOFAC. Amesema China ni mshirika mkubwa wa Tanzania anayetegemewa na asiyekosekana. Chama cha Mapinduzi cha Tanzania CCM kina urafiki wa kindugu na Chama cha Kikomunisti cha China, na Tanzania inapenda kutumia vyema Chuo cha Uongozi cha Nyerere ili kuongeza mafunzo ya kujenga chama na kubadilishana uzoefu katika utawala wa nchi na China, na kuendelea kupanua ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali. Amesisitiza kuwa Tanzania inathamini sana pendekezo lililotolewa na Rais Xi Jinping la kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na inafurahi kushuhudia ufufukaji wa Reli ya TAZARA katika ziara hii.
Katika mkutano huo, China na Tanzania zimetia saini nyaraka kadhaa za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika maeneo kama vile utandawazi wa miundombinu na biashara ya mazao ya kilimo.