Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema karibu kesi 367 za Mpox, ikiwemo vifo vitatu, vimethibitishwa katika nchi tano za kusini na mashariki mwa Afrika, huku kukiwa na wasiwasi kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.
Ofisi hiyo imesema, mpaka kufikia jumatatu wiki hii, Burundi imerekodi kesi 328 za Mpox, Afrika Kusini kesi 24, Uganda kesi saba na Rwanda na Kenya kesi nne kila moja.
Ofisi ya OCHA kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu ugonjwa huo, kwamba zaidi ya kesi 3,800 za Mpox zimethibitishwa barani Afrika tangu mwezi Januari mwaka huu, huku Burundi ikiwa ni nchi ya pili kuathiriwa zaidi katika bara hilo baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ugonjwa huo kuwa dharura ya afya ya kimataifa na kutoa wito wa mwitikio ulioratibiwa wa kimataifa kuzuia mlipuko wa Mpox na kuokoa maisha.