Aliyejiteka apate pesa atiwa mbaroni
2024-09-05 23:11:20| cri

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limemtia mbaroni Ramadhani Shaban, 21, mkazi wa Buronge Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa wazazi wake kwamba ametekwa ili kuwezesha ndugu zake kutoa fedha kwa watekaji aweze kukombolewa.

Sambamba na mtuhumiwa huyo polisi pia inawashikilia watu wawili Kassimu Kibona na Ramadhani Issa ambapo mtu huyo alikuwa akishirikiana nao kujificha (kujiteka) hadi fedha kiasi cha Sh milioni 2.5 zitolewe ili waweze kumkomboa.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma Filemon Makungu alisema kuwa wakati polisi wakiendelea na upelelezi Ramadhani alifikishwa na wazazi wake kituo kikuu cha polisi Mkoa Kigoma wakieleza kuwa amepatikana eneo la Msimba Dampo nje kidogo ya Manispaa ya Kigoma Ujiji baada ya kutoa fedha kwa watekaji.

Polisi imeeleza kuwa uchunguzi wa kina walioufanya umegundua kuwa watuhumiwa walitoa taarifa za uongo kwa nia ya kujipatia fedha na hivyo kuwatia mbaroni ambapo wanatarajia kufikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.