Mkimbiaji wa mbio za Marathon Rebecca Cheptegei, ambaye alilazwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, (MTRH) Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, nchini Kenya amefariki dunia.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MTRH Dkt Owen Menach, ambaye ni mkurugenzi wa huduma za kliniki na upasuaji amesema, Cheptegei ambaye alilazwa katika chumba cha dharura (ICU), alikufa saa 11 asubuhi kutokana na kile alichoelezea kama viungo vyote kushindwa kufanya kazi.
"Inasikitisha kwamba tumempoteza mgonjwa mapema asubuhi ya leo baada ya viungo vyake vyote kushindwa kufanya kazi saa 11 asubuhi wakati tulikuwa tunafanya bidii kuokoa maisha yake," Dk Menach alisema.
Mgonjwa alikuwa na majeraha ya moto kwa asilimia 80 na alifungwa badeji karibu mwili mzima kwa sababu ya kuungua na alikuwa akisaidiwa kuwekewa damu, maji, dawa na kupumua.
Cheptegei, mwenye umri wa miaka 33, aliungua vibaya kutokana na makali ya moto baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na aliyekuwa mpenzi wake.