Rais Xi Jinping akutana na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame
2024-09-06 08:27:34| CRI

Rais Xi Jinping wa China jana usiku katika Jumba Kuu la Mikutano ya Umma mjini Beijing alikutana na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame ambaye yuko China kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).



Rais Xi amesema China inaiunga mkono Rwanda kufuata njia ya maendeleo inayojitegemea na kujiamulia, na inapenda kubadilishana uzoefu na Rwanda kuhusu utawala wa nchi na chama, kuzidisha kuaminiana kisiasa, kupanua maoni ya pamoja na kusonga mbele bega kwa bega katika njia ya kuelekea kuwa nchi za kisasa.



Rais Xi amesisitiza kuwa, China inapenda kushirikiana na Rwanda katika kutekeleza matokeo ya mkutano huo, kukuza ushirikiano katika nyanja za miundombinu, kilimo na matumizi ya satelaiti, kuendesha vizuri Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Rwanda na Karakana ya Luban, na kuhimiza ushirikiano wa nchi hizo mbili katika ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” uzae matunda mengi zaidi.



Kwa upande wake, Rais Kagame amesema Rwanda itafuata kithabiti sera ya kuwepo kwa China moja duniani, inaiunga mkono China kutimiza umoja wa taifa, msimamo ambao umejengwa katika msingi wa urafiki na maelewano kati ya nchi hizo mbili. Amesisitiza kuwa, Rwanda inaichukulia China kama rafiki na mshirika wa kuaminika, na inapenda kupanua ushirikiano na China katika nyanja mbalimbali, na kutekeleza kwa pamoja mapendekezo matatu kuhusu maendeleo, usalama na ustaarabu wa dunia yaliyotolewa na Rais Xi.