Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema China imekuwa mshirika wa kweli katika maendeleo ya Afrika, na ushirikiano kati ya Afrika na China utasaidia kujenga maendeleo ya pamoja na ustawi wa siku zijazo.
Akihutubia ufunguzi wa Mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika jana mjini Beijing, rais Samia amesema, nchi za Afrika zinathamini sana hatua 10 za ushirikiano kati ya China na Afrika zilizotangazwa na rais Xi Jinping wa China ili kukuza kwa pamoja ujenzi wa mambo ya kisasa.
Pia rais Samia amesema, biashara na uwekezaji kati ya nchi za Afrika na China zimekua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, na kuongeza kuwa, Tanzania iko tayari kuwa jukwaa la mfano la ushirikiano wa uvumbuzi wa kiuchumi na kijamii kati ya Afrika na China.