Wataalamu wamekutana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kujadili njia za kutangaza suluhisho la matumizi ya teknolojia za kifedha ili kuboresha biashara ya ndani ya bara la Afrika.
Toleo la 11 la Mkutano wa Teknolojia ya Kifedha wa Afrika umekutanisha zaidi ya washiriki 200 wakiwemo maofisa waandamizi wa serikali na sekta ya huduma za kifedha kutoka Afrika ili kutathmini njia za kupanua matumizi ya teknolojia za kidijitali kuimarisha biashara kati ya nchi za Afrika.
Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) Wamkele Mene, amesema teknolojia ya kifedha ni moja ya njia za kuongeza kiwango cha maingiliano ya kibiashara ndani ya Afrika, ambayo inakadiriwa kuwa ni asilimia 15 ikilinganishwa na asilimia 70 ya Umoja wa Ulaya na asilimia 60 barani Asia.
Naye Katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali nchini Kenya, John Tanui, amesema teknolojia ya kifedha inatoa fursa nyingi kuliko utaratibu wa kawaida wa kibenki kutokana na kuwa na suluhisho la kivumbuzi la kidijitali linalowezesha malipo ya papo kwa hapo ya kuvuka mpaka.